KUZA MAISHA YAKO
KWA KUFUGA BATA MZINGA
Ufugaji wa bata
mzinga ni njia bora na rahisi sana kwa mfugaji yeyote aliyetayari kukuza kipato
chake kwa haraka sana na kwa kiwango cha juu.
Bata
mzinga ni jamii ya ndege wafugwao majumbani na wanaotaga mayai kama kuku ama
bata.
Ndege hawa ni
wakubwa sana, kichwa chao hakina manyoya na kina rangi nyekundu, pinki au
kijivu. Manyoya yao pia yana rangi nyeusi au nyeupe na yenye madoa
yanayometameta.
Watu
wengi huwafananisha sana na mbuni, lakini tofauti yao ni kwamba, shingo ya bata
mzinga siyo ndefu sana kama ya mbuni, wana nyama inayoning’inia kutoka shingoni
na manyoya yaliyoning’inia shingoni ambapo mara nyingi huchanua na kuwa kama
shanga.
Ndege
hawa pia wana mkia mrefu kiasi na huchanua kama tausi lakini siyo ndefu sana.
Kutaga na
kutamia
Bata
dume humpanda na kumng’ata jike kwa muda mrefu sana, na humuachia pindi jike
anapotoa ute ute kama wa ng’ombe lakini ni mwepesi kiasi. Wakati mwingine
unaweza kuhisi anamuua kwani jike hulia sana.
Hapo
jike anakuwa tayari kutaga na hutaga mayai 15 hadi 17 kwa mara ya kwanza na
kisha hutamia. Anapoendelea kukua huweza kutaga hadi mayai 30 (hii hulingana na
lishe nzuri atakayopatiwa).
Mayai
ya bata mzinga hutamiwa kwa siku 28 na huanza kuanguliwa vifaranga kwa muda wa
siku 3, kuanzia siku ya siku ya 28 na hadi 31. Baada ya hapo mayai hutakiwa
kutupwa kwa kuwa hayatoanguliwa tena.
Bata
mzinga hutamia mayai kuanzia 17 hadi 20 (kama ni yake kutokana na ukubwa),
lakini kama ni ya kuku basi huweza kutamia mayai 30.
Unaweza
kumuwekea kuku au bata mayai ya bata mzinga na akatamia na kuangua vifaranga
vya bata mzinga kwa siku 28 tu.
Utunzaji wa vifaranga
na chakula
Wachukue
vifaranga pamoja na mama yao na kuwaweka kwenye banda safi lisilopitisha baridi
kisha kuwawekea taa. Banda lako liwe limesakafiwa, au banda la asili la udongo.
Pia waweza kutumia banda lenye mbao au mabanzi kwa chini na katika mabanda yako
waweza kuweka soda ili kuwakinga na baridi.
Chukua
mahindi 5kg (yasiyokuwa na dawa), karanga 5kg, dagaa 5kg, mashudu 10kg, chokaa
5kg pamoja na mayai ya kuku yaliyochemshwa na kupoa 3, kisha twanga au saga
pamoja na kuwalisha. Mchanganyiko huu hutegemeana na wingi wa bata mzinga
unaowafuga (hakikisha kila bata anapata chakula cha kutosha lakini mchanganyiko
ufuate uwiano huo). Hakikisha unawaangalia mara kwa mara kama wanachakula kwani
bata mzinga huwa hawaiti vifaranga wake kula kama kuku afanyavyo.
Chukua
maji na wawekee katika chombo ambacho hawatamwaga na wanakifikia vizuri.
Kumbuka kuwa wakimwaga maji banda litachafuka na magonjwa mengi ni rahisi
kuibuka.
Kama
hali ni nzuri kifedha, waweza kununua chakula kilichosagwa tayari kwa ajili ya
vifaranga (stata) na uwape kwa muda wa wiki sita kisha waweza kuwapatia vyakula
vingine kama mahindi yasiyosagwa na hata dagaa zisizosagwa kwani watakuwa
tayari wanaweza kula kama bata mzinga wakubwa.
Pia
ni vizuri ukawalisha bata mzinga vyakula vingine kama majani ambayo huwapatia
protini (kunde, fiwi na majani mengine jamii ya mikunde).
Kumbuka
kuwa bata mzinga watakula sana ikiwa unawafungia, hivyo ni lazima kuhakikisha
unawapatia chakula cha kutosha chenye virutubisho vya aina zote pamoja na maji.
Magonjwa
Bata
mzinga hushambuliwa na magonjwa kama kuku na mara wanapougua ni rahisi sana
kuambukiza kuku na bata wengine kwa haraka sana.
Magonjwa
yanayowasumbua sana ni typhoid, mafua na kuharisha damu. Pia husumbuliwa sana
na viroboto wanaosababishwa na uchafu wa banda hasa kuwa na vumbi. Viroboto hao
hupelekea kunyonyoka kwa manyoya ya bata mzinga wakati wa kujikuna na hatimaye
kufa.
Tiba za asili
Waweza
kuwatibu vifaranga au bata mzinga wako kwa kutumia njia ya asili ambayo pia ni
rahisi, gharama nafuu na bora zaidi kuliko kutumia madawa yaliyochanganywa na
kemikali na yenye gharama.
Vifuatazo
ni vitu vya asili vinavyotumika kutibu magonjwa mbali mbali kwa bata mzinga na
yanayopatikana kwa wingi katika maeneo ya mfugaji. Madawa haya hutumika kwa
kiwango cha wastani na hayana kipimo maalum kwani hata ukiyazidisha hayana
madhara.
·
Mwarobaini na
Aloe Vera:
Madawa haya hutumika kutibu kuharisha
damu pamoja na mafua kwa vifaranga vya bata mzinga. Chukua kiasi kidogo cha
mwarubaini kisha twanga vizuri kupata maji maji. Kamua maji yale, kisha weka
katika maji uliyoandaa kuwanywesha vifaranga wako. Kata vipande vidogovidogo vya aloe vera (jani moja laweza kutosha) na
tia katika maji yaliyochanganywa na mwarobaini, kisha wapatie vifaranga wanywe
(Aloe Vera itaendelea kujikamua yenyewe ikiwa ndani ya maji huku vifaranga
wakiendele kunywa).
·
Kitunguu swaumu: Hii hutumika kukinga
na kutibu vifaranga vya bata mzinga wanaosumbuliwa na kuharisha damu. Unachukua
kitunguu swaumu na kuondoa maganda ya nje kisha kusafisha na kukata vipande
vidogo sana, na kuwawekea kama chakula. Vifaranga wanapenda sana vitunguu hivyo
na watakula kwa kasi kama chakula lakini ni tiba tayari. Unaweza kuwapatia kila
siku hadi watakapo pona.
·
Maziwa:Maziwa yanayotokana
na ng’ombe pia hutumika kutibu ugonjwa wa kuhara damu pamoja na kuwapa nguvu
bata mzinga waliolegea. Mnyweshwe maziwa hayo bata anayeumwa bila kuyachemsha
na umnyweshe maziwa ya kutosha kiasi cha kushiba. Unamnywesha mara tatu kwa
siku. Hakikisha maziwa unayotumia yanatoka kwa ng’ombe wanaotibiwa kila mara.
·
Majani: Bata Mzinga
hupendelea sana kula majani na ni chakula chao kikuu. Majani yana vitamini A,
hivyo ni vyema kuwalisha bata bzinga kila siku ili kuhakikisha unawapatia
vitamini ya kutosha.
Angalizo
Siyo
lazima bata mzinga waugue ndipo uwapatie tiba hizi. Hakikisha unawapa tiba
kabla hata hawajaugua hivyo utawakinga na magonjwa hayo. Waweza kuchanganya
madawa hayo yote kwa wakati mmoja kwani hayana madhara.
Endapo
madawa ya asili hayapatikani katika eneo la mfugaji basi waweza kuwatibu bata
mzinga kwa madawa yafuatayo ambapo vipimo huelezwa moja kwa moja kwa maandishi
katika madawa hayo au kuelezwa na muuzaji pale utakaponunulia;
Amprolium
kwa ugonjwa wa kuharisha damu (Coccidiosis), Fluban,Coridix au Doxyco
kutibu mafua (Coryza) na Esb3,Trisulmycine
au Trimazine. Hii dawa hutumika kwa homa ya matumbo (Typhoid).
Chanjo
Bata
mzinga wanatakiwa kupatiwa chanjo ya ndui(mara moja kila mwaka), kideri(kila
baada ya miezi mitatu), gomboro(kwa muda wa wiki tano)ukiwapa jumatatau, basi
unawapatia kila jumatatu ya wiki) na vitamini A mara baada ya kuanguliwa.
Usafi
Bata
Mzinga tofauti na ndege wa aina nyingine wanaofugwa, wanaasili ya usafi na hawapendi
kukaa sehemu zenye uchafu, tope wala mizoga, tofauti na bata.
Mara
nyingi wanapoona mwenzao kashusha mabawa na kanyong’onyea, basi bata wengine hupanda
juu ya mgongo wake na kumkanyaga kanyaga huku wakimdonoa hadi kufa.
Kwa
maana hiyo, hakikisha banda lao ni safi kila mara na unawaangalia bata kila
baada ya masaa nawili. Unapogundua kuna mwenye dalili za kuumwa basi mtenge na
wenzake na kumtibu.
Ni
muhimu kusafisha banda lao mara tatu kwa wiki kwani ndege hawa hujisaidia kwa
wingi na mara nyingi uchafu wao ni mwingi na una umajimaji kama vile kuhara.
Soko
Bata
mzinga mmoja huwa na kilo kuanzia 12 hadi 20 huku dume akiwa na kilo kati ya 25
hadi 35. Hii ni kwa wastani wa bata mzinga wanaopatiwa matunzo na lishe ya
kutosha.
Soko
la bata mzinga liko juu sana kwa mayai na nyama. Bata mzinga pia hutofautiana bei
kwa jike na dume (walaji wengi hupenda bata mzinga dume).
Bata
mzinga jike anaweza kuuzwa kati ya shilingi 150,000 hadi 200,000, lakini dume huuzwa
kati ya shilingi 200,000 hadi shilingi 300,000. Bei hizi huwa nzuri zaidi katika
miezi ya Novemba na Disemba.
Mayai
yake pia huuzwa kwa bei nzuri sana. Yai moja huuzwa kuanzia 8,000 hadi 12,000 kwa
wakati wowote ule.
Faida
Mbali
na kipato cha juu, bata mzinga wana faida nyinginezo kama zifuatazo;
Bata
mzinga hutamia na kutotoa vifaranga wa ndege wengine kama kuku, bata, kanga na
hata kwale. Pia si rahisi mayai yanayofunikwa na bata mzinga kuwa maji ama
kutoanguliwa kwani huyafunika vizuri na hapendi kutoka nje hovyo (ana mabawa
makubwa yatakayofunika mayai vizuri na kutoa joto la kutosha).
Ndege
huyu ni mlinzi kwa binadamu wakati wowote hasa wakati wa usiku kwani adui
anapopita karibu na eneo lake hata kama ni binadamu, bata mzinga hulia sana.
Bata
mzinga huweza kutamia mayai ya kuku thelathini na kuyaangua yote na hufunika
vifaranga kwa kiwango hicho bila hata mmoja kuonekana nje(kutokana na ukubwa wa
mabawa yake).
Bata
mzinga hutamia mara nne kwa mwaka (kila baada ya miezi mitatu)bila shida yeyote
na waweza kumuuza akiwa na miezi sita hadi nane kwa bei nzuri kabisa.
Ni
rahisi pia kumtofautisha kati ya duma na jike wakiwa bado wadogo kutoka na
sababu kuwa, bata mzinga dume hunyanyua mabawa yake kila wakati na hutoa sauti
fulani, hii itakusaidia endapo utahitaji kuwatenga dume na jike kwa kuwatunza
katika mabanda tofauti.
Kwa maelezo
zaidi kuhusu bata mzinga, unaweza kuwasiliana na Solomon Kingalame, mtaalamu wa
ufugaji na mzalishaji wa vifaranga vya bata mzinga kwa simu namba 0762 183856,
au mfugaji Victoria S.Lekamoy kwa simu namba 0767423201.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment