KITUNGUU
SAUMU MKOMBOZI WA UCHUMI NA AFYA
Kitunguu
swaumu (Garllic) ni zao lenye manufaa sana kiafya na katika kuinua kipato cha
mkulima. Ulimaji wake hauna gharama kubwa endapo litalimwa kwa kuzingatia
wakati na eneo stahiki.
Zao hili ni miongoni
mwa viungo muhimu vya chakula hapa nchini na vinavyotumika kwa wingi. Aidha,
zao hili limepata umaarufu mkubwa katika kuweka harufu kwenye chakula muhimu
sana hapa Tanzania (pilau) na kinachopendwa na wengi katika sikukuu mbalimbali.
Ingawa wengi hukitumia kuongeza harufu kwenye chakula hicho bado hawajafahamu manufaa
yake kiafya na kiuchumi.
Historia inaonyesha
kuwa, vitunguu saumu vilianza kutumika China mwaka 510 K.K na pia vilitumiwa na
wanajeshi wa Ugiriki na Roma. Zao hili pia lilianza kutumika katika maabara
mbalimbali duniani hususani Asia, Afrika na Ulaya takribani miaka 6000
iliyopita. Matumizi makuu nyakati hizo yakiwa viungo katika mboga na tiba.
Kutokana na viasilia
mbalimbali vinavyopatikana katika zao hili na zinazofanya kazi tofauti,
zimeisaidia kuwa na uwezo na faida nyingi katika mwili wa binadamu hasa
kutumika kama kinga na tiba ya maradhi mbalimbali.
Udongo
Kitunguu saumu huota
zaidi ukanda wa juu kuanzia mita 900 hadi 1500. Pia huota katika udongo wa aina
yeyote lakini hustawi zaidi katika udongo usiotuamisha maji. Udongo huo ni
lazima uwe na mbolea ya kutosha hasa ya asili.
Ikiwa udongo wako ama
ardhi unayotumia kuotesha kitunguu chako haina mbolea ya kutosha basi hakikisha
unaurutubisha kwa kuweka mboji ama samadi iliyoozeshwa vizuri. Pia waweza
kuweka samadi mbichi iliyotoka moja kwa moja zizini katika shamba lako kisha
kulilima huku ukichanganya samadi na udongo vizuri na kuliacha kwa muda wa
miezi saba hadi kumi kisha kulilima tena na kuotesha vitunguu vyako.
Mbolea za viwandani
kama Ammonium Sulphate, Ammonium Nitrate, DAP, Urea na nyingine zaweza kutumika
kwa kiwango kitakachoshauriwa na wataalamu wa kilimo na kwa muda sahihi japo
hatukushauri sana kuitumia kwani mbolea ya samadi pekee yatosha.
Hali
ya hewa
Kwa nchi ya Tanzania,
zao hili huoteshwa na kusitawi vizuri katika kipindi ambacho joto ama ni la
wastani. Iwe ni kipindi cha baridi japo si baridi sana (Nyuzi joto 18C hadi
22C).
Utayarishaji
wa shamba
Hakikisha shamba lako
lipo katika eneo zuri lisilotuamisha maji na lisafishe vizuri kwa kuondoa
magugu yote na kisha kuyafukia kwani ni rutuba pindi yakioza. Weka mboji na
kisha lilime vizuri kwa kuchanganya mbole na udongo tayari kwa kuotesha.
Utayarishaji
wa mbegu
Vitunguu vinavyoota
vizuri ni vile vilivyohifadhiwa sehemu nzuri isiyokuwa na unyevu, na katika
eneo lenye joto la wastani. Kama utahifadhi katika sehemu yenye joto jingi na
hakuna hewa ya kutosha basi ukiviotesha vitunguu hivyo vitazalisha mavuno duni
na dhaifu.
Kabla ya kupeleka
shambani, chukua kitunguu saumu na kuchambua kwa kutenganisha vitunguu kimoja
kimoja kisha kuchagua vile vitunguu vikubwa kwa kuwa hivi ndivyo
vitakavyokupatia mavuno mengi na vitunguu vyenye ubora, kisha peleka shambani
tayari kwa kuotesha.
Namna
ya kuotesha
Piga mashimo kama ya
kuoteshea maharage. Nafasi kati ya mche na mche iwe ni sentimeta 8-12 na kati
ya mstari na mstari iwe ni sentimeta 25-30 (visiwe mbalimbali kama kitunguu
maji kwani vitunguu swaumu havinenepi sana na unapootesha karibu ndipo
unapokuwa na kiwango kikubwa cha mavuno.
Weka kitunguu chako
katika mashimo ukihakikisha kuwa mizizi inakuwa chini na shina linaangalia juu.
Hakikisha vitunguu vyako haviegemei upande wowote bali vimesimama wima.
Baada ya kuweka katika
mashimo, fukia kwa udongo wa kutosha na uukandamize kwa nguvu kiasi ili
kuhakikisha kitunguu chako kimekaa vizuri na hakiwezi kuanguka ama kuathiriwa
na kitu chochote kama kung’olewa na mvua au maji wakati wa kumwagilia. Pia kwa
kufanya hivyo utakinga mazao yako kuharibiwa na wanyama kama mbwa wakati
wakikatisha na hata kuingia katika shamba lako.
Kuchipua
Baada ya siku kumi hadi
siku kumi na sita, kitunguu swaumu kitachipua na kuanza kutoa majani hadi kumi
na sita. Jani la katikati ambalo litaweka mbegu, litaendelea kukua na kupita
majani mengine kwa urefu (mbegu hiyo ni kitunguu na huwa ni kimoja tu, lakini
utakapokiotesha baada ya kuvuna kitaota na kuzaa vitunguu vingine vingi).
Umwagiliaji
Kwa kipindi cha mvua,
huna haja kabisa kumwagilia kwani maji ya mvua tayari yanatosha. Kama ni
kipindi cha kiangazi hakikisah unamwagilia vitunguu vyako kila unapoona shamba
limekauka. Unaweza kumwagilia mara mbili hadi tatu kwa wiki.
Usimwagilie vitunguu
wakati wa mchana au jioni. Ni vizuri sana kumwagilia wakati wa asubuhi ili
kuipa uwezo wa kupambana na magonjwa kwani wakati kama wa jioni utaongeza uwezo
wa vitunguu kushambulia na barafu na hata kuoza.
Uwe na utaratibu wa
kuchunguza vitunguu vyako kama vimezaliana vya kutosha hasa baada ya miezi
miwili kwa kuchimba kidogo. Ukishagundua kuwa vimezaliana vizuri, usimwagilie
tena bali viache na kuipa nafasi kukomaa kwani ukiendelea na umwagiliaji basi
vitunguu vyako vitaoza.
Usafi
wa shamba
Mara zote shamba lako
linahitajika kuwa safi kwa kilimo bora. Hakikisha unafanya usafi kwa kung’oa
magugu na majani yasiyohitajika ili kuondoa ushindani baina yake na vitunguu
vyako ambavyo vitakuwa vikigombea rutuba, hewa na maji.
Ni muhimu sana kufanya
palizi walau mara nne hadi tano kufikia mavuno.
Magonjwa
Kama ilivyo kwa mazao
mengi ya bustani, kitunguu saumu hushambuliwa na magonjwa kama ukungu, kuoza,
fangas pamoja na wadudu.
Namna
ya kuondokana na magonjwa hayo
Ni muhimu sana
kudhibiti magonjwa haya mara tu uonapo dalili kwa kutumia viuatilifu ili
kuondokana na hasara kubwa itakayotokea.
Unatakiwa pia kufanya
kilimo cha mzunguko wa mazao katika shamba lako yasiyo jamii moja ya vitunguu saumu
kama kuotesha mahindi, maharage ili kuondokana na magonjwa mengine ambayo
yanaweza kuwa sugu.
Pia, kuepukana na
umwagiliaji wa jioni na usiku pamoja na kuotesha katika maeneo yanayotuamisha
maji kutasaidia kuzuia ugonjwa wa kutu kwenye majani na fangas.
Ikiwa mimea tayari
imevamiwa na ugonjwa wa kutu, basi mimea yote ing’olewe na kuchomwa ili
kuinginga mimea ijayo itakayooteshwa katika shamba hilo.
Kukomaa
hadi kuvuna
Kitunguu swaumu
huchukua miezi mitatu na nusu hadi minne kukomaa. Utagundua kuwa kitunguu chako
kimekomaa na kipo tayari kuvunwa mara baada ya jani lake dogo la mwisho
litakapokauka. Hapo watakiwa kuingia shambani na kuvuna.
Namna
ya kuhifadhi
Mara baada ya kuving’oa
vitunguu vyako, na majani yake yakiwa bado mabichi, chukua kamba na funga
mafundo ya ukubwa kiasi (Unafunga kwenye majani), kisha vining’inize juu katika
eneo lenye joto la wastani (kusiwe na unyevu wala ubaridi). Vitunguu vyako
vitaendelea kukauka taratibu huku vikinyonya yale maji yote yaliyopo kwenye
majani yake.
Pia waweza kuvikata
majani na kupunguza mizizi baada ya kung’oa kisha kuweka darini na vitaendelea
kukauka taratibu.
Kama ulitumia mbolea ya
samadi au mboji, waweza kuhifadhi kitunguu chako kwa muda wa miezi saba hadi
nane bila kuharibika na ikiwa umetumia mbolea za viwandani basi vitunguu vyako
vyaweza kuharibika baada ya miezi mitatu au minne.
Faida
za kitunguu saumu kiafya
Kutokana na tafiti
mbalimbali zilizofanywa na wanasayansi kama Louis Pasteur, kitunguu swaumu
kimegundulika kuwa na uwezo wa kutibu na kukinga magonjwa mengi yanayomsumbua
binadamu kila wakati.
Imegundulika kuwa
kitunguu saumu husaidia kuzuia maradhi ya saratani pamoja na malaria kutokana
na kemikali ambazo hutoka baada ya kukata ama wakati wa kutafuna.
Uchunguzi umebaini kuwa
kitunguu saumu huweza kupunguza athari za kemikali nyingine zisizofaa mwilini
hasa zitokanazo na moshi na kuimarisha uwezo wa seli za mwili.
Mwaka 1845,
mwanasayansi Pasteur aligundua kuwa kitunguu swaumu huweza kutumika kama tiba
ya vidonda na huzuia donda ndugu kwa kiasi kikubwa.
Haikuishia hapo,
kitunguu saumu pia hutumika kama tiba ya mafua, kuzuia magonjwa ya moyo kwa
kupungua kiwango cha lijamu, kupunguza shinikizo la damu na kurekebisha kiwango
cha sukari mwilini.
Mwisho
No comments:
Post a Comment