Thursday, March 20, 2014

FAHAMU MAAJAMU YA KITUNGUU SWAUMU KWA AFYA YAKO



KITUNGUU SAUMU MKOMBOZI WA UCHUMI NA AFYA
Kitunguu swaumu (Garllic) ni zao lenye manufaa sana kiafya na katika kuinua kipato cha mkulima. Ulimaji wake hauna gharama kubwa endapo litalimwa kwa kuzingatia wakati  na eneo stahiki.

Zao hili ni miongoni mwa viungo muhimu vya chakula hapa nchini na vinavyotumika kwa wingi. Aidha, zao hili limepata umaarufu mkubwa katika kuweka harufu kwenye chakula muhimu sana hapa Tanzania (pilau) na kinachopendwa na wengi katika sikukuu mbalimbali. Ingawa wengi hukitumia kuongeza harufu kwenye chakula hicho bado hawajafahamu manufaa yake kiafya na kiuchumi.
Historia inaonyesha kuwa, vitunguu saumu vilianza kutumika China mwaka 510 K.K na pia vilitumiwa na wanajeshi wa Ugiriki na Roma. Zao hili pia lilianza kutumika katika maabara mbalimbali duniani hususani Asia, Afrika na Ulaya takribani miaka 6000 iliyopita. Matumizi makuu nyakati hizo yakiwa viungo katika mboga na tiba.

Kutokana na viasilia mbalimbali vinavyopatikana katika zao hili na zinazofanya kazi tofauti, zimeisaidia kuwa na uwezo na faida nyingi katika mwili wa binadamu hasa kutumika kama kinga na tiba ya maradhi mbalimbali.

Udongo
Kitunguu saumu huota zaidi ukanda wa juu kuanzia mita 900 hadi 1500. Pia huota katika udongo wa aina yeyote lakini hustawi zaidi katika udongo usiotuamisha maji. Udongo huo ni lazima uwe na mbolea ya kutosha hasa ya asili.

Ikiwa udongo wako ama ardhi unayotumia kuotesha kitunguu chako haina mbolea ya kutosha basi hakikisha unaurutubisha kwa kuweka mboji ama samadi iliyoozeshwa vizuri. Pia waweza kuweka samadi mbichi iliyotoka moja kwa moja zizini katika shamba lako kisha kulilima huku ukichanganya samadi na udongo vizuri na kuliacha kwa muda wa miezi saba hadi kumi kisha kulilima tena na kuotesha vitunguu vyako.

Mbolea za viwandani kama Ammonium Sulphate, Ammonium Nitrate, DAP, Urea na nyingine zaweza kutumika kwa kiwango kitakachoshauriwa na wataalamu wa kilimo na kwa muda sahihi japo hatukushauri sana kuitumia kwani mbolea ya samadi pekee yatosha.

Hali ya hewa
Kwa nchi ya Tanzania, zao hili huoteshwa na kusitawi vizuri katika kipindi ambacho joto ama ni la wastani. Iwe ni kipindi cha baridi japo si baridi sana (Nyuzi joto 18C hadi 22C).


Utayarishaji wa shamba
Hakikisha shamba lako lipo katika eneo zuri lisilotuamisha maji na lisafishe vizuri kwa kuondoa magugu yote na kisha kuyafukia kwani ni rutuba pindi yakioza. Weka mboji na kisha lilime vizuri kwa kuchanganya mbole na udongo tayari kwa kuotesha.

Utayarishaji wa mbegu
Vitunguu vinavyoota vizuri ni vile vilivyohifadhiwa sehemu nzuri isiyokuwa na unyevu, na katika eneo lenye joto la wastani. Kama utahifadhi katika sehemu yenye joto jingi na hakuna hewa ya kutosha basi ukiviotesha vitunguu hivyo vitazalisha mavuno duni na dhaifu.

Kabla ya kupeleka shambani, chukua kitunguu saumu na kuchambua kwa kutenganisha vitunguu kimoja kimoja kisha kuchagua vile vitunguu vikubwa kwa kuwa hivi ndivyo vitakavyokupatia mavuno mengi na vitunguu vyenye ubora, kisha peleka shambani tayari kwa kuotesha.

Namna ya kuotesha
Piga mashimo kama ya kuoteshea maharage. Nafasi kati ya mche na mche iwe ni sentimeta 8-12 na kati ya mstari na mstari iwe ni sentimeta 25-30 (visiwe mbalimbali kama kitunguu maji kwani vitunguu swaumu havinenepi sana na unapootesha karibu ndipo unapokuwa na kiwango kikubwa cha mavuno.

Weka kitunguu chako katika mashimo ukihakikisha kuwa mizizi inakuwa chini na shina linaangalia juu. Hakikisha vitunguu vyako haviegemei upande wowote bali vimesimama wima.
Baada ya kuweka katika mashimo, fukia kwa udongo wa kutosha na uukandamize kwa nguvu kiasi ili kuhakikisha kitunguu chako kimekaa vizuri na hakiwezi kuanguka ama kuathiriwa na kitu chochote kama kung’olewa na mvua au maji wakati wa kumwagilia. Pia kwa kufanya hivyo utakinga mazao yako kuharibiwa na wanyama kama mbwa wakati wakikatisha na hata kuingia katika shamba lako.

Kuchipua
Baada ya siku kumi hadi siku kumi na sita, kitunguu swaumu kitachipua na kuanza kutoa majani hadi kumi na sita. Jani la katikati ambalo litaweka mbegu, litaendelea kukua na kupita majani mengine kwa urefu (mbegu hiyo ni kitunguu na huwa ni kimoja tu, lakini utakapokiotesha baada ya kuvuna kitaota na kuzaa vitunguu vingine vingi).

Umwagiliaji
Kwa kipindi cha mvua, huna haja kabisa kumwagilia kwani maji ya mvua tayari yanatosha. Kama ni kipindi cha kiangazi hakikisah unamwagilia vitunguu vyako kila unapoona shamba limekauka. Unaweza kumwagilia mara mbili hadi tatu kwa wiki.

Usimwagilie vitunguu wakati wa mchana au jioni. Ni vizuri sana kumwagilia wakati wa asubuhi ili kuipa uwezo wa kupambana na magonjwa kwani wakati kama wa jioni utaongeza uwezo wa vitunguu kushambulia na barafu na hata kuoza.

Uwe na utaratibu wa kuchunguza vitunguu vyako kama vimezaliana vya kutosha hasa baada ya miezi miwili kwa kuchimba kidogo. Ukishagundua kuwa vimezaliana vizuri, usimwagilie tena bali viache na kuipa nafasi kukomaa kwani ukiendelea na umwagiliaji basi vitunguu vyako vitaoza.

Usafi wa shamba
Mara zote shamba lako linahitajika kuwa safi kwa kilimo bora. Hakikisha unafanya usafi kwa kung’oa magugu na majani yasiyohitajika ili kuondoa ushindani baina yake na vitunguu vyako ambavyo vitakuwa vikigombea rutuba, hewa na maji.
Ni muhimu sana kufanya palizi walau mara nne hadi tano kufikia mavuno.

Magonjwa
Kama ilivyo kwa mazao mengi ya bustani, kitunguu saumu hushambuliwa na magonjwa kama ukungu, kuoza, fangas pamoja na wadudu.

Namna ya kuondokana na magonjwa hayo
Ni muhimu sana kudhibiti magonjwa haya mara tu uonapo dalili kwa kutumia viuatilifu ili kuondokana na hasara kubwa itakayotokea.

Unatakiwa pia kufanya kilimo cha mzunguko wa mazao katika shamba lako yasiyo jamii moja ya vitunguu saumu kama kuotesha mahindi, maharage ili kuondokana na magonjwa mengine ambayo yanaweza kuwa sugu.

Pia, kuepukana na umwagiliaji wa jioni na usiku pamoja na kuotesha katika maeneo yanayotuamisha maji kutasaidia kuzuia ugonjwa wa kutu kwenye majani na fangas.
Ikiwa mimea tayari imevamiwa na ugonjwa wa kutu, basi mimea yote ing’olewe na kuchomwa ili kuinginga mimea ijayo itakayooteshwa katika shamba hilo.


Kukomaa hadi kuvuna
Kitunguu swaumu huchukua miezi mitatu na nusu hadi minne kukomaa. Utagundua kuwa kitunguu chako kimekomaa na kipo tayari kuvunwa mara baada ya jani lake dogo la mwisho litakapokauka. Hapo watakiwa kuingia shambani na kuvuna.

Namna ya kuhifadhi
Mara baada ya kuving’oa vitunguu vyako, na majani yake yakiwa bado mabichi, chukua kamba na funga mafundo ya ukubwa kiasi (Unafunga kwenye majani), kisha vining’inize juu katika eneo lenye joto la wastani (kusiwe na unyevu wala ubaridi). Vitunguu vyako vitaendelea kukauka taratibu huku vikinyonya yale maji yote yaliyopo kwenye majani yake.

Pia waweza kuvikata majani na kupunguza mizizi baada ya kung’oa kisha kuweka darini na vitaendelea kukauka taratibu.

Kama ulitumia mbolea ya samadi au mboji, waweza kuhifadhi kitunguu chako kwa muda wa miezi saba hadi nane bila kuharibika na ikiwa umetumia mbolea za viwandani basi vitunguu vyako vyaweza kuharibika baada ya miezi mitatu au minne.

Faida za kitunguu saumu kiafya
Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na wanasayansi kama Louis Pasteur, kitunguu swaumu kimegundulika kuwa na uwezo wa kutibu na kukinga magonjwa mengi yanayomsumbua binadamu kila wakati.

Imegundulika kuwa kitunguu saumu husaidia kuzuia maradhi ya saratani pamoja na malaria kutokana na kemikali ambazo hutoka baada ya kukata ama wakati wa kutafuna.

Uchunguzi umebaini kuwa kitunguu saumu huweza kupunguza athari za kemikali nyingine zisizofaa mwilini hasa zitokanazo na moshi na kuimarisha uwezo wa seli za mwili.

Mwaka 1845, mwanasayansi Pasteur aligundua kuwa kitunguu swaumu huweza kutumika kama tiba ya vidonda na huzuia donda ndugu kwa kiasi kikubwa.

Haikuishia hapo, kitunguu saumu pia hutumika kama tiba ya mafua, kuzuia magonjwa ya moyo kwa kupungua kiwango cha lijamu, kupunguza shinikizo la damu na kurekebisha kiwango cha sukari mwilini.
Mwisho


Why no work on this?



KUZA MAISHA YAKO KWA KUFUGA BATA MZINGA
Ufugaji wa bata mzinga ni njia bora na rahisi sana kwa mfugaji yeyote aliyetayari kukuza kipato chake kwa haraka sana na kwa kiwango cha juu.
Bata mzinga ni jamii ya ndege wafugwao majumbani na wanaotaga mayai kama kuku ama bata.
Ndege hawa ni wakubwa sana, kichwa chao hakina manyoya na kina rangi nyekundu, pinki au kijivu. Manyoya yao pia yana rangi nyeusi au nyeupe na yenye madoa yanayometameta.  
Watu wengi huwafananisha sana na mbuni, lakini tofauti yao ni kwamba, shingo ya bata mzinga siyo ndefu sana kama ya mbuni, wana nyama inayoning’inia kutoka shingoni na manyoya yaliyoning’inia shingoni ambapo mara nyingi huchanua na kuwa kama shanga.
Ndege hawa pia wana mkia mrefu kiasi na huchanua kama tausi lakini siyo ndefu sana.
Kutaga na kutamia
Bata dume humpanda na kumng’ata jike kwa muda mrefu sana, na humuachia pindi jike anapotoa ute ute kama wa ng’ombe lakini ni mwepesi kiasi. Wakati mwingine unaweza kuhisi anamuua kwani jike hulia sana.
Hapo jike anakuwa tayari kutaga na hutaga mayai 15 hadi 17 kwa mara ya kwanza na kisha hutamia. Anapoendelea kukua huweza kutaga hadi mayai 30 (hii hulingana na lishe nzuri atakayopatiwa).
Mayai ya bata mzinga hutamiwa kwa siku 28 na huanza kuanguliwa vifaranga kwa muda wa siku 3, kuanzia siku ya siku ya 28 na hadi 31. Baada ya hapo mayai hutakiwa kutupwa kwa kuwa hayatoanguliwa tena.
Bata mzinga hutamia mayai kuanzia 17 hadi 20 (kama ni yake kutokana na ukubwa), lakini kama ni ya kuku basi huweza kutamia mayai 30.
Unaweza kumuwekea kuku au bata mayai ya bata mzinga na akatamia na kuangua vifaranga vya bata mzinga kwa siku 28 tu.
Utunzaji wa vifaranga na chakula
Wachukue vifaranga pamoja na mama yao na kuwaweka kwenye banda safi lisilopitisha baridi kisha kuwawekea taa. Banda lako liwe limesakafiwa, au banda la asili la udongo. Pia waweza kutumia banda lenye mbao au mabanzi kwa chini na katika mabanda yako waweza kuweka soda ili kuwakinga na baridi.
Chukua mahindi 5kg (yasiyokuwa na dawa), karanga 5kg, dagaa 5kg, mashudu 10kg, chokaa 5kg pamoja na mayai ya kuku yaliyochemshwa na kupoa 3, kisha twanga au saga pamoja na kuwalisha. Mchanganyiko huu hutegemeana na wingi wa bata mzinga unaowafuga (hakikisha kila bata anapata chakula cha kutosha lakini mchanganyiko ufuate uwiano huo). Hakikisha unawaangalia mara kwa mara kama wanachakula kwani bata mzinga huwa hawaiti vifaranga wake kula kama kuku afanyavyo.
Chukua maji na wawekee katika chombo ambacho hawatamwaga na wanakifikia vizuri. Kumbuka kuwa wakimwaga maji banda litachafuka na magonjwa mengi ni rahisi kuibuka.
Kama hali ni nzuri kifedha, waweza kununua chakula kilichosagwa tayari kwa ajili ya vifaranga (stata) na uwape kwa muda wa wiki sita kisha waweza kuwapatia vyakula vingine kama mahindi yasiyosagwa na hata dagaa zisizosagwa kwani watakuwa tayari wanaweza kula kama bata mzinga wakubwa.
Pia ni vizuri ukawalisha bata mzinga vyakula vingine kama majani ambayo huwapatia protini (kunde, fiwi na majani mengine jamii ya mikunde).
Kumbuka kuwa bata mzinga watakula sana ikiwa unawafungia, hivyo ni lazima kuhakikisha unawapatia chakula cha kutosha chenye virutubisho vya aina zote pamoja na maji.
Magonjwa
Bata mzinga hushambuliwa na magonjwa kama kuku na mara wanapougua ni rahisi sana kuambukiza kuku na bata wengine kwa haraka sana.
Magonjwa yanayowasumbua sana ni typhoid, mafua na kuharisha damu. Pia husumbuliwa sana na viroboto wanaosababishwa na uchafu wa banda hasa kuwa na vumbi. Viroboto hao hupelekea kunyonyoka kwa manyoya ya bata mzinga wakati wa kujikuna na hatimaye kufa.
Tiba za asili
Waweza kuwatibu vifaranga au bata mzinga wako kwa kutumia njia ya asili ambayo pia ni rahisi, gharama nafuu na bora zaidi kuliko kutumia madawa yaliyochanganywa na kemikali na yenye gharama.
Vifuatazo ni vitu vya asili vinavyotumika kutibu magonjwa mbali mbali kwa bata mzinga na yanayopatikana kwa wingi katika maeneo ya mfugaji. Madawa haya hutumika kwa kiwango cha wastani na hayana kipimo maalum kwani hata ukiyazidisha hayana madhara.
·         Mwarobaini na Aloe Vera: Madawa haya hutumika kutibu  kuharisha damu pamoja na mafua kwa vifaranga vya bata mzinga. Chukua kiasi kidogo cha mwarubaini kisha twanga vizuri kupata maji maji. Kamua maji yale, kisha weka katika maji uliyoandaa kuwanywesha vifaranga wako. Kata vipande vidogovidogo  vya aloe vera (jani moja laweza kutosha) na tia katika maji yaliyochanganywa na mwarobaini, kisha wapatie vifaranga wanywe (Aloe Vera itaendelea kujikamua yenyewe ikiwa ndani ya maji huku vifaranga wakiendele kunywa).
·         Kitunguu swaumu: Hii hutumika kukinga na kutibu vifaranga vya bata mzinga wanaosumbuliwa na kuharisha damu. Unachukua kitunguu swaumu na kuondoa maganda ya nje kisha kusafisha na kukata vipande vidogo sana, na kuwawekea kama chakula. Vifaranga wanapenda sana vitunguu hivyo na watakula kwa kasi kama chakula lakini ni tiba tayari. Unaweza kuwapatia kila siku hadi watakapo pona.
·         Maziwa:Maziwa yanayotokana na ng’ombe pia hutumika kutibu ugonjwa wa kuhara damu pamoja na kuwapa nguvu bata mzinga waliolegea. Mnyweshwe maziwa hayo bata anayeumwa bila kuyachemsha na umnyweshe maziwa ya kutosha kiasi cha kushiba. Unamnywesha mara tatu kwa siku. Hakikisha maziwa unayotumia yanatoka kwa ng’ombe wanaotibiwa kila mara.
·         Majani: Bata Mzinga hupendelea sana kula majani na ni chakula chao kikuu. Majani yana vitamini A, hivyo ni vyema kuwalisha bata bzinga kila siku ili kuhakikisha unawapatia vitamini ya kutosha.
Angalizo
Siyo lazima bata mzinga waugue ndipo uwapatie tiba hizi. Hakikisha unawapa tiba kabla hata hawajaugua hivyo utawakinga na magonjwa hayo. Waweza kuchanganya madawa hayo yote kwa wakati mmoja kwani hayana madhara.
Endapo madawa ya asili hayapatikani katika eneo la mfugaji basi waweza kuwatibu bata mzinga kwa madawa yafuatayo ambapo vipimo huelezwa moja kwa moja kwa maandishi katika madawa hayo au kuelezwa na muuzaji pale utakaponunulia;
Amprolium kwa ugonjwa wa kuharisha damu (Coccidiosis), Fluban,Coridix au Doxyco kutibu  mafua (Coryza) na Esb3,Trisulmycine au Trimazine. Hii dawa hutumika kwa homa ya matumbo (Typhoid).  
Chanjo
Bata mzinga wanatakiwa kupatiwa chanjo ya ndui(mara moja kila mwaka), kideri(kila baada ya miezi mitatu), gomboro(kwa muda wa wiki tano)ukiwapa jumatatau, basi unawapatia kila jumatatu ya wiki) na vitamini A mara baada ya kuanguliwa.
Usafi
Bata Mzinga tofauti na ndege wa aina nyingine wanaofugwa, wanaasili ya usafi na hawapendi kukaa sehemu zenye uchafu, tope wala mizoga, tofauti na bata.
Mara nyingi wanapoona mwenzao kashusha mabawa na kanyong’onyea, basi bata wengine hupanda juu ya mgongo wake na kumkanyaga kanyaga huku wakimdonoa hadi kufa.
Kwa maana hiyo, hakikisha banda lao ni safi kila mara na unawaangalia bata kila baada ya masaa nawili. Unapogundua kuna mwenye dalili za kuumwa basi mtenge na wenzake na kumtibu.
Ni muhimu kusafisha banda lao mara tatu kwa wiki kwani ndege hawa hujisaidia kwa wingi na mara nyingi uchafu wao ni mwingi na una umajimaji kama vile kuhara.
Soko
Bata mzinga mmoja huwa na kilo kuanzia 12 hadi 20 huku dume akiwa na kilo kati ya 25 hadi 35. Hii ni kwa wastani wa bata mzinga wanaopatiwa matunzo na lishe ya kutosha.
Soko la bata mzinga liko juu sana kwa mayai na nyama. Bata mzinga pia hutofautiana bei kwa jike na dume (walaji wengi hupenda bata mzinga dume).
Bata mzinga jike anaweza kuuzwa kati ya shilingi 150,000 hadi 200,000, lakini dume huuzwa kati ya shilingi 200,000 hadi shilingi 300,000. Bei hizi huwa nzuri zaidi katika miezi ya Novemba na Disemba.
Mayai yake pia huuzwa kwa bei nzuri sana. Yai moja huuzwa kuanzia 8,000 hadi 12,000 kwa wakati wowote ule.

Faida
Mbali na kipato cha juu, bata mzinga wana faida nyinginezo kama zifuatazo;
Bata mzinga hutamia na kutotoa vifaranga wa ndege wengine kama kuku, bata, kanga na hata kwale. Pia si rahisi mayai yanayofunikwa na bata mzinga kuwa maji ama kutoanguliwa kwani huyafunika vizuri na hapendi kutoka nje hovyo (ana mabawa makubwa yatakayofunika mayai vizuri na kutoa joto la kutosha).
Ndege huyu ni mlinzi kwa binadamu wakati wowote hasa wakati wa usiku kwani adui anapopita karibu na eneo lake hata kama ni binadamu, bata mzinga hulia sana.
Bata mzinga huweza kutamia mayai ya kuku thelathini na kuyaangua yote na hufunika vifaranga kwa kiwango hicho bila hata mmoja kuonekana nje(kutokana na ukubwa wa mabawa yake).
Bata mzinga hutamia mara nne kwa mwaka (kila baada ya miezi mitatu)bila shida yeyote na waweza kumuuza akiwa na miezi sita hadi nane kwa bei nzuri kabisa.
Ni rahisi pia kumtofautisha kati ya duma na jike wakiwa bado wadogo kutoka na sababu kuwa, bata mzinga dume hunyanyua mabawa yake kila wakati na hutoa sauti fulani, hii itakusaidia endapo utahitaji kuwatenga dume na jike kwa kuwatunza katika mabanda tofauti.
Kwa maelezo zaidi kuhusu bata mzinga, unaweza kuwasiliana na Solomon Kingalame, mtaalamu wa ufugaji na mzalishaji wa vifaranga vya bata mzinga kwa simu namba 0762 183856, au mfugaji Victoria S.Lekamoy kwa simu namba 0767423201.
Mwisho.